HISTORIA YETU
Huduma ya maji katika mji wa Songea ilianzishwa mnamo mwaka 1950.Chanzo kikuu cha maji kilikuwa ni kutoka mto Ruvuma ambapo ililenga kuhudumia wakazi wapatao 5,000 waliokuwa wanaishi katika mji wa songea wakiwa na wastani wa meta za ujazo 400 kwa siku. Kwa wakati huo huduma hii ilikuwa ikisimamiwa na serikali kuu chini ya Idara ya Maji.Kufuatia ongezeko la watu mjini Songea, ubora wa huduma ulizidi kupungua mwaka hadi mwaka.
Mnaomo mwaka 1997 Serikali ilianzisha utaratibu mpya wa kusimamia huduma hii ya Majisafi na Uondoaji wa Maji taka kwa lengo la uboreshaji.
Kwa hiyo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ziliundwa kwaajili ya Miji, Manispaa na Majiji nchini Tanzania,ikiwemo Manispaa ya Songea.
Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira Manispaa ya Songea ilianzishwa tarehe 01-07-1997 kwa sheria Namba 8 ya mwaka 1997 ambayo imeridhiwa na Sheria namba 12 ya mwaka 2009. Wakati inaanzishwa Mamlaka ilikuwa chini ya bodi ya ushauri na baadae hapo tarehe 01-01-1998 ilianza kufanya kazi chini ya bodi ya Wakurugenzi. Mpaka sasa mamlaka hii iko daraja "A" la Mamlaka za Majisafi na usafi wa Mazingira Mjini,Tanzania Bara ambayo inajitegemea kwa gharama zote isipokuwa uwezekazaji mkubwa ambao unafanywa na Serikali Kuu. Ili kujiendesha Mamlaka inategemea makusanyo ya fedha kutoka kwa wateja wanaopatiwa huduma ya Majisafi na Uondoaji wa Majitaka.